Skip to main content

HAKI YA WANYONGE



MNYONGE ATAWAHI KUPATA HAKI?

Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na kilio kisichoonekana kupungua huku  wananchi wakikumbana na dhiki kuu wakiumia kutokana na janga la mahangaiko na taabu  chungu nzima, chanzo chake kikiwa ni hawa mabepari walio miongoni mwetu. Huku wakenya-wananchi wa kawaida  wakiendelea kupitia shida kila uchao, wengine wao wakilazimika kujitia kitanzi kutokana na hali ngumu ya maisha, wengine wanaamua kuingia katika vikundi vya magaidi ambavyo vinawaahidi vikapu vinono vinono punde baanda ya kutekeleza ‘kazi’, mabwanyenye wenye mali kama njugu wanaendelea kutajirika hata zaidi. Si ajabu wala kusikitisha kusema kuwa mabwanyenye wawa hawa ni ndugu na jamaa zetu, marafiki na wendani wetu kindakindaki. Ni watu tuliowaaminia sana katika baadhi ya mambo yetu ya kimaisha.
Watu wengi wanaoishi katika mitaa ya mabanda wanakumbana na changamoto  tofautitofauti, nyingi yazo zikiwa ni pamoja na ukosefu wa chakula cha kutosha, uhaba wa maji safi ya kunywa na ya matumizi ya kijumla ya pale nyumbani, magonjwa(kama vile saratani, kipindupindu na malaria), ukosefu wa makaazi ya kutosha, mazingira machafu, hali inayotishia sana afya ya wapendwa hawa. Yahuzunisha sana kuwaona mavijulanga wakifilia mahospitalini, wengine wakikauka na kuzimia mikononi mwa mama zao pale nyumbani kwa ukosefu wa matibabu na dawa. Katika habari za hivi majuzi, wengi wa wananchi hawa wa kawaida wamelazimika sasa kuelekeza matumaini yao kwa wale madaktari gushi ambao hawakuhitimu kuitwa madaktari na hivyo kuwapa wagonjwa madawa ambayo pia ni gushi ambayo hulenga kuyaangamiza maisha ya watu hawa wasokuwa na hatia. Watu wengi sasa wamejiingiza  katika biashara za kuuza madawa na wamefungua vioski vingi ambavyo wanaviita kliniki. Wanatoa  huduma kwa bei nafuu mno ikilinganishwa na zile hospitali na zahanati na umma ambazo zina leseni na idhini ya kutenda kazi. Kutokana na uhaba wa fedha ndipo hawa wananchi wenye matumaini finyu hulazimika kwenda katika hivi vijikioski ili kutafuta msaada. Pongezi tele kwa huduma ya afya kwa kujitokeza tisti na kukabiliana na swala hili.
Uhai wa mwanadamu ni jambo nyeti sana ambalo lafaa kuangaliwa kwa makini zaidi kuliko kitu chochote kile. Madaktari na mataabibu gushi wafaa kung’atuliwa kwenye huu ulingo wa matibbu ili usalama wa afya ya watu  wetu unahakikishiwa.   
Swala hili la vijana kuanza kujihusisha na kujiingiza katika mambo ya kigaidi, huku wakiyahatarisha maisha wa wananchi wa dhamani limekuwa ni kero miongoni mwa wengi wa mamilioni ya wakenya. Kwanza, ikizingatiwa kuwa hali ya maisha kwa sasa imekuwa ngumu kutokana na uhaba wa ajira miongoni mwa vijana, wakiwemo wale waliosoma na kuhitimu na shahada zao katika vyuo. Ni aibu kubwa sana kukariri kuwa wapo wale viongozi walaghai, wenye mifuko ya kaburi na wenye matumbo yasiyoshiba kama jehanamu ambao huyanyoosha mikono yao katika ile hazina iliyotengewa vijana ili kuwasaidia katika kuwapa ajira na kudukua pesa hizo kisha kujilimbikizia katika akaunti zao. Na unapowapata katika mikutano na kusanyiko kule minadani, wanajipiga vifua wakieleza vile walivyo na mioyo ya huruma ya kuwasaidia wananchi wa kawaida na kuzipigania haki zao, wakitoa ahadi za kuwainua vijana kutoka vuli la mauti ya ukosefu ajira. Jambo ambalo wengi wamesema miaka nenda miaka rudi lakini hakuna tunda hata moja lililochipuka.

Ugatuzi ulipotangulizwa katika nchi yetu hii mnamo mwaka wa 2013, wakenya walikuwa na matarajio chungu nzima, jambo ambalo liliwasha taa ya matumaini miongoni mwa wananchi wa kawaida  kwani mfumo huu ulikuja na vifurushi vya mambo mazuri mazuri. Wananchi wangepata huduma zao moja kwa moja kutoka kwa serikali ya jimbo(Kaunti). Huduma za afya sasa zingeboreshwa na wananchi wa kawaida wangepata fursa ya kuyapata matibabu kwa bei nafuu, madawa ya kutosha, vifaa vya umatibabu vya kutosha, malazi ya kutosha mle hospitalini kwa wagonjwa na akina mama wanaoelekea kujifungua.

Kinaya cha haya yote yalionekana pale ambapo simba walianza kuonyesha kucha zao ndefu! Kwa muktadha wa hali halisia ya siku hizi, kuna visa vingi vya wanawake au watoto kufia hospitalini wakati wa  kufifungua, watu wanaaga dunia wakipokea matibabu mahospitalini. Halikadhalika kumekuwa na visa si haba vinavyosuhusu wananchi kulalamikia uhaba/ na ukosefu wa dawa za kutosha katika hospitali na zahanati za umma, jambo ambalo limezua kero kubwa katika serikali ya kitaifa. Si ajabu kudokeza kuwa wapo madaktari na wale wanaojihusisha na huduma za matibabu kulaghai dawa zinazopaswa kupewa wagonjwa ili ziwape afueni, na bila aibu wanazisafirisha kimagendo katika kliniki zao za binafsi huku wakiwaacha wananchi wakijifilia kama nzi.  Isitoshe, vyakula vya wagonjwa mle hospitalini huchezewa karata na kuhepeshwa kijanja sana hadi nyumba za hawa wahudumu wa afya. Wananenepa na kumetameta huku maskini hohehahe wakibaki katika hali za ukiwa usiku na mchana. Je, huu ni ungwana? Je, huu ni utu, au uhayawani?
Ninapopita katika mitaa kila mara hukumbana na vikundi vya watoto wa umri changa kabisa, wengi wao ni wadogo sana kuwa katika mazingira kama yale! Mitaa yetu imesheheni machokoraa kotekote. Wanatembea hapa na pale wakitafuta angaa ganda la muwa uliotafunwa hadi utamu wote kuisha ili apigane na janga la njaa lililomkaba barabara. Mara mingi utawapata wamejilaza kama magogo kwenye veranda za maduka kila asubuhi unapopita. Wengine wana nguo zilizochanika na kuwa kama tambara la kupangusia miguu mlangoni. Wamekonda na kukondeana, uzi kando na ni wenye afya zilizodhoofika kwelikweli.
Katika pitapita zangu katika mtaa wa Majengo, Githurai 45, nilikutana na genge  hili la vijana wa mitaani wakipunga unyunyu katika maskani yao, ambayo huiita ‘Base’. Na baada ya mazungumzo ya ana kwa ana na baadhi yao nilipata habari zilizonikwaruza moyo.

Baadhi yao walijipata mitaani wakiwa machokora kutokana na sababu za kusikitisha, zingine zikiwa ni za kukera moyo sana. Nilipigwa na bumbuwazi nilipowaona hata akina dada wakiwa miongoni wa genge lile, wao pia wakilibingirisha    gurudumu hili la maisha ya mitaani. Kunao waliotoroka kwao nyumbani kutokana na vita na migogoro ya mashamba kati ya wazazi wao na mababe wa mji/ kijiji. Mashamba yao yalinyakuliwa kwa  mabavu na hivyo basi, mnyonge hana haki… Walikosa wa kuwatetea na kuwasaidia kupigania haki zao. Wakajikuta mitaani. Wengine wao  akina dada walidhulumiwa kimapenzi na vijiume vya mitaa na kutupwa kama tambara bovu huku wakiachwa na simanzi isiyokuwa na kifani. Wengine ni kutokana tu na hali ngumu zaidi ya maisha kule vijijini mwao ndiposa wakajikuta mitaani. Cha ajabu sana ni kukutana na wale waliokuwa wanafunzi vyuoni na kuhitimu na shahada zao pia wakilisukuma gurudumu lili hili la maisha hapa mtaani. Wametafuta ajira miaka nenda miaka rudi, wameibisha milango ya ofisi karibu zote kuomba nafasi za ajira wakiwa na imani kuwa kwa vile wamehitimu, watapata kazi zinazotosheleza shahada zao. Lakini wakashindwa kufua dafu kwani wana majina yasiyopatikana katika kabila la mkurugenzi, ama ana kisomo cha kiwango cha juu zaidi kuliko cha meneja. Hali hii huwaacha katika bahari ya luja wakifikiria la kufanya na pa kuenda wasione.
Ni wazi kukariri kuwa tumeambukizwa na hivyo kuugua kutokana na ugonjwa sugu wa ufisadi na ukabila. Bila kuzingatia tajiriba na kiwango cha masomo ya mtu mtafutakazi, wakubwa katika afisi za umma wanawachagua watu wa jamaa na kabila  zao ambao wengine wao hawahitimu kuingia katika kazi fulani. Uadilifu haupo tena. Milungula inaliwa tokea vijijini hadi mijini. Kila mtu anaangalia tumbo lake na kuwasahau wenye njaa zaidi kumliko yeye.
     
Kwa hivyo, ni ulimwengu tunaosihi ndani mwake. Watu wamekosa uadilifu na kuwa kama wanyama wa porini wasiomezeana mate. Wanyonge wameachwa bila sauti za kujitetea na kupigania haki zao. Dunia ya leo kinachojalisha tu ni kuwa bora una pesa na mali nyingi ndiposa utakubaliwa na jamii yenye tabaka la juu. Haijalishi una maoni mazito kiasi gani. Asiyekuwa nacho kamwe hana la kusema ila ni kimya kimtawale. Na wale walionavyo kila mara ni kuwanyanyasa na kuwadhulumu wasionavyo.  

Ninapotia kikomo katika makala haya, ningependa kutoa maoni yangu, kulingana na mtazamo wangu juu ya ukengeufu tulio nao kama Waafrika ni kuwa bado hatujajielewa sisi ni akina nani. Tumesahau kuwa kabla hatujajinyakulia uhuru mnamo mwaka wa 1963 December, tulikuwa watumwa wa Mabepari Wakoloni na tuliwafanyia kazi kutwa kucha bila kuchoka kwa mishahara ya kijungu jiko. Wakati mwingine hatukulipwa ila kwa makonde na matusi. Mashamba yetu yalinyakuliwa kwa nguvu na watoto na waume  wetu kupelekwa matekani. Wake zetu nao hawakusazwa ng’o! Haki zetu tulinyimwa na hapakuwa na wa kututetea. Hali hii ilibaadilika wakati akili zetu zilifunguka na tukawa na wazo la kupigania uhuru wetu. Kisha tukawa na mashujaa waliojitolea mhanga kuyapoteza maisha yao kwa kusudi la kulipa taifa uhuru. Damu ilimwagika na wengi wakaachwa bila makao. Kwa hivyo, ni mengi yalitukia na ulikuwa  mchakato mrefu sana, lakini sitaki kwenda huko kwa sasa. Cha mno ni kuwa wakati huo tulikuwa na umoja. Tulizungumza lugha moja, tukawa na wazo moja, sauti moja na maono sawa. Tulipendana kama halua na satua na utamaduni huu ndio ulitupelekea sisi kupata uhuru hatimaye.
Baaada ya nchi yetu kupata uhuru tulifurahia matunda ya kung’ang’ana kwetu na kuahidiana mmoja kwa mwingine kuwa hatutamwona mmoja wetu akidhulumiwa na tuketi kitako huku tukitazama. Ilikuwa eti tupendane na kujali jirani. Yanayotendeka sasa ni kinaya cha haya yote kwani maadili yameporomoka mioyoni mwa wanadamu Waafrika. Nilidhani tutapendana na kubebeana mizigo mmoja kwa mwingine wakati wa msiba, kama tu tulivyoagana…ukiwa na utu basi huwezi kumdhulumu msichana mdogo kimapenzi na kumtupa kama kopo la msalani. Unatarajia ataishi namna gani? Hiyo mimba uliyompachika endapo atamzaa mtoto. Je, atamtunza vipi kwanza ikizingatiwa kuwa wewe ndiwe unawajibika? Ashakum si matusi, lakini watu kama hawa ni sharti wachululiwe hatua kali sana za kisheria ili kukomesha kizungu hiki.









Makala na: Otieno Calleb O.
07-14-531-574
Nairobi, Kenya.               

Comments