Skip to main content

MAISHA YA CHUO



MAISHA YA CHUO  

Kwa kawaida, kazi nzuri na bidii hupelekea matokeo kabambe na mwishowe fanaka maishani. Hii huwa ndiyo hali kwa wanafunzi wanaofanya mtiani wao wa wa kitaifa, KCSE ambapo wengine wao hufuzu na kujishindia nafasi katika vyuo vikuu ili kusomea kozi ambazo zinawafaa zaidi. Huu ndio wakati utawapata wana na binti za watu wakizikokota begi nzito nzito ardhini huku wanatembea kwa ustaha na ujarisi wakielekea chuoni, nyuso zao zikimetameta metumetu kwa tabasamu ya furaha. Hiki ndicho kiwango ambacho humezewa mate na wengi wa watahiniwa wa KCSE na  kila mmoja hujinyima usingizi na starehe ili kupigania fursa hii. Wengi wanaojiunga na vyuo huwa na matarajio mengi kuhusu maisha na mustakabali wao baada ya masomo ya chuo. Wao huwa na mtazamo dhabiti katika masomo yao na kamwe hawataruhusu upuuzi wowote uuondoe umakinifu wao kutoka kwa ‘kazi’ waliyokuja kuifanya mle chuoni. 

Awali katika shule za upili, wengi huwa na maono makubwa makubwa ya kuwa madaktari, wahandisi, meneja, marubani, wapasuaji wakuu, mahakimu, wakili,wafanyibiashara wakubwa  na kozi nyingine zenye mishahara nono nono. Cha kustaajabisha mno ni kuwa utasikia wachache sana wakitaja ualimu au hata ukose…Haya basi. Mambo hubadilika punde tu wanapopokea matokeo yao ya KCSE. Hivyo, wao hujiunga na vyuo na kufanya zile kozi zinazooana na ‘grades’ zao.

Wageni chuoni

Chuo hujaa pomoni na wanafunzi kutoka pande zote za taifa. Wapo wanaotoka vijijini, mijini na wale wenye heri walioishi jijini kama nyumbani kwao halisi. Katika kutambua mazingira mapya na geni kabisa, wanafunzi huzunguka kote kote chuoni kwa vikundi huku wakipiga selfie na kufurahia kuwa chuoni. Wengine huandaa sherehe, ‘Bash’ ambapo huwaalika marafiki zao kutoka vyuo vingine, ndugu na jamaa zao ili waje wawasaidie kuidhinisha siku ile na kuifanya yenye fanaka na kumbukumbu. 

Hapa ndipo wanafunzi limbukeni hupata fursa murwa ya kujifunza mambo mageni ya mjini, teknolojia mpya na kuanza kuona mambo ambayo hawajawahi kuyaona maishani mwao tangu kuzaliwa. Vyumba vyenye zulia nyekundu, sakafu za mawe ya dhamani, vyoo vya kisasa, milango yenye vijidude vya kutomaswa kisha vinasonga vyenyewe,  na mambo mengine mengi ambayo huwaacha achama, ila kujisimamisha kadamnasi ya vyombo hivi ili angaa wapige picha ambayo watawapelekea jamaa zao nyumbani watakaporudi likizoni. Papa hapa ndipo wanakutana na ghorofa zenye lifti ambazo hutenda kazi kama daladala kwa kutomasa vijidude ukutani ili kuiamurisha ikushushe katika ghorofa ambayo ungependa. Halikadhalika, hapa ndipo wengine wao hujigundua kuwa kumbe bado wako nyuma katika mtindo wa mavazi na hivyo basi kuanza kuiga mitindo ya mavazi ya wale ‘wazee’ wa chuo. Maongezi pia yanabadilika katika awamu hii maana ni wakati wa kujigundua. Wengi uhujiunga na vyama malimbali huku wakifanya urafiki na wenzao.
Wengi hupotea njia. Hasa sana ikipatikana  kuwa chuo ni kikubwa na pana. Si ajabu baadhi ya vyuo huwapa wanafunzi wapya ramani ya chuo punde wanapoingia ili iwasaidie kupata kumbi za mafunzo, idara mahususi na afisi ambazo wangependa kutembelea. Licha ya hayo, kunao wengine ambao bado hupotea njia na kutokana na hili, hufika katika kumbi za mihadhara wakiwa wamechelewa au wakose kabisa kupata ukumbi hivyo basi kukosa kuhudhuria mhadhara. Wajuaji nao hufurahia na kujivunia ujuaji wao. 

Mijarabu na mitihani 

Huu huwa ni wakati wa kubaini mbivu na bichi. Wahadhiri wa vyuo huwapa wanafunzi takribani mijarabu miwili, moja ukiwa ni wa kufanyia utafiki na kuwasilishwa kama kazi ya muhula, huku nyingine hupeanwa darasani na wanafunzi huifanya kama mtihani. Mambo huwaharibikia wale ambao waliponda raha ya Campus na kukosa kuhudhuria mihadhara na kusoma halikadhalika. Wengine hulazimika kutumia mbinu zisizo halali kujinyakulia alama nene.
Msukumo mwingi hutokea hasa nyakati za mtihani wa mswisho wa muhula. Utawaona wanafunzi wakifululiza(kwa msururu mrefu) maktabani asubuni na mapema, hata Jumapili. Wengine vitabu vi mikobani, wengine wamevining’iniza viganjani na kutembea aste aste, vichwa wamevisimamisha wima angani. Sitaki nikueleze yale hutukia mle maktabani wakiwa wamezingirwa na furushi ya vitabu vya kila aina. Mezani pametandikwa  vitabu vikubwa vikubwa huku mengine yamesimamishwa kwenye kingo za meza, nusra vianguke. Watu wanasoma!
Nyakati za mitihani, utawapata wengine bado wangali na vijitabu kwenye barabara za kuelekea kwenye kumbi za mitihani wakijaribu kuguguna maneno chinichini na kuyakariri mara kadhaa kama kibwagizo cha shairi arudhi.
Baada ya mitihani ya mwinso wa muhula watu hurudi kwao nyumbani kuungana na jamii zao baada ya miaezi mitatu. 

 Maisha ya chuo

Chuoni utayastaajabia ya Musa. Ya Firauni pia utayaona vilevile kwani ni mahali penye sura ya karakana ya jua kali. Utakutana na chochote, utakumbana na mtu yeyote. Changamoto nazo ni chungu nzima. Lakini utafanyani? Wahenga walisema kuwa dunia ni uwanja wa fujo. Maisha ni jani kavu, linateketezwa motoni kisha halipo tena. Wapo wanafunzi waliotoka katika familia tajiri na wenye mali kama mchanga baharini. Kwa upande kinyume, kuna wale waliotoka katika aila hohehahe wanaoishi maisha ya kiganja na mdomo. Wana mapato  finyu.
Walio navyo kila mara watataka kuonyesha kuwa kwa kweli wanavyo. Na maskini pia hawatakuwa na budi kutafuta namna ya kujikimu, hivyo kuwalazimisha kujihusisha katika shughuli mbalimbali za kutafuta namna. Wengine hulazimika kutafuta ajira katika makampuni mjini ili angaa wapate jinsi ya kukamilisha karo ya chuo, kulipa kodi ya nyumba na kujikimu kimaisha. Wengine hulazimika kujiingiza katika ulingo wa biashara ambapo huuza nguo za mitumba, vyatu na matunda katika mitaa ya chuo. Wengine hufungua vyumba vya kuonyeshea sinema. Watu hufanya mambo mengi tu ambayo huwasaidia kujikimu maishani. Si ajabu kuwa wengine wataingia katika biashara zisizo halali kama za kuuza dawa za kulevya na mali nyingi nyingine gushi.
Kwa wale walio na heri, maisha kwao ni kama mswaki. Kila kitu wanachohitaji wanacho. Kwa namna hii, wengi huwa wazembe sana hasa katika kufanya kazi zao za muhula na hivyo kuwalipa wale wenye akili walio na mahitaji ya pesa ili kurahisisha kazi. Ni mengi hutukia na hii yote husababishwa na swala kuwa hakuna wa kumchunga mwanafunzi kama ilivyokuwa katika shule za upili. 

Iwapo unatarajia kujiunga na chuo, ama wewe ni mzazi una mtoto ambaye ungependa kumwingiza chuoni hivi karibuni, basi haya ni baadhi tu yay ale hutukia mle chuoni. Zingatia ukweli kuwa wapo wanaoenda chuoni wakiwa na matumaini mengi maishani ya kufanikiwa na hivyo basi huwa na bidii za mchwa katika mtalaa wao lakini hapo katikati mambo hubadilika na kuwageukia. Maisha yanawakazia kamba na wanachoweza kufanya ni kusalimu amri za kuingia katika ulimwengu tayari kwa mapambano.  

Comments