MAISHA YA CHUO Kwa kawaida, kazi nzuri na bidii hupelekea matokeo kabambe na mwishowe fanaka maishani. Hii huwa ndiyo hali kwa wanafunzi wanaofanya mtiani wao wa wa kitaifa, KCSE ambapo wengine wao hufuzu na kujishindia nafasi katika vyuo vikuu ili kusomea kozi ambazo zinawafaa zaidi. Huu ndio wakati utawapata wana na binti za watu wakizikokota begi nzito nzito ardhini huku wanatembea kwa ustaha na ujarisi wakielekea chuoni, nyuso zao zikimetameta metumetu kwa tabasamu ya furaha. Hiki ndicho kiwango ambacho humezewa mate na wengi wa watahiniwa wa KCSE na kila mmoja hujinyima usingizi na starehe ili kupigania fursa hii. Wengi wanaojiunga na vyuo huwa na matarajio mengi kuhusu maisha na mustakabali wao baada ya masomo ya chuo. Wao huwa na mtazamo dhabiti katika masomo yao na kamwe hawataruhusu upuuzi wowote uuondoe umakinifu wao kutoka kwa ‘kazi’ waliyokuja kuifanya mle chuoni. Awali katika shule za upili, wengi huwa na maono makubwa makubwa ya kuwa ...